Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete, akimpa shada la
maua Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, ikiwa ni kumpongeza mbunge
huyo nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana.Picha: Tryphone Mweji
Baada ya Spika, Anne Makinda, kutaja jina la Ridhiwani, wabunge wengi walilipuka kwa shagwe na vigelegele tofauti na ilivyokuwa kwa Mgimwa na baada ya kuapishwa kwao, wabunge wengi walikwenda kumpongeza Ridhiwani.
Bila kujali shughuli za Bunge zilizokuwa zikiendelea, wabunge hao wakiwamo baadhi ya mawaziri, walikwenda kwanza kumpongeza Ridhiwani licha ya Mgimwa kuwa wa kwanza kwenye eneo walilokaa.
Hali hiyo ilionekana kumkera Spika Makinda baada ya wabunge kuendelea kumpongeza Ridhiwani hata baada ya shughuli ya kuwaapisha kumalizika na shughuli nyingine za Bunge kuendelea na kulazimika kutoa angalizo kwao.
“Waheshimiwa wabunge na mawaziri, naomba tutulie, kwa kwenda kumpongeza tunavunja kanuni," alisema Makinda, hatua iliyowalazimisha na wabunge na mawaziri kurudi kwenye nafasi zao.
Vile vile, Spika Makinda alikemea tabia ya baadhi ya wabunge wanawake kushangilia kwa kupiga vigelegele na kuwaeleza kuwa hayo yanafanyika katika Bunge Maalum la Katiba na siyo kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano.
”Hapa mnashangilia kwa kupiga makofi ya kibunge na siyo vigelegele, hayo yanafanyika kwenye Bunge Maalum la Katiba, msilete masuala ya Bunge lile kwenye Bunge hili, lazima mfuate kanuni za Bunge hili,” aliongeza.
Makinda alitoa kauli hiyo baada ya kumtambulisha mke wa Rais, Salma Kikwete, aliyefika kwenye ukumbi wa Bunge hilo kushuhudia kuapishwa kwa
Ridhiwani.
Baada ya kauli hiyo, wabunge walitulia na kushangilia kwa kupiga makofi.
Nje ya Bunge, Salma alimpokea Ridhiwani kwa shangwe na kumpa ua kama ishara ya pongezi huku wabunge wengi wakimshangilia Ridhiwani zaidi na Mgimwa kuonekana mpweke.
Aidha, Mgimwa hakupewa maua makubwa na mengi kama Ridhiwani na wabunge wengi walipigana vikumbo kumsalimu Salma.
Ridhiwani na Mgimwa, waliapishwa na Makinda ambaye alianza kwa kumwapisha Mgimwa saa 3:10 asubuhi na kufuatiwa na Ridhiwani saa 3:13 asubuhi.
Kundi la wabunge wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walifuatana na wabunge hao kwa kuimba nyimbo na vigelegele hadi eneo maalum la kuapia na baada ya kuapishwa walisalimiana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na wabunge wengine na kwa upande wa upinzani, walisalimiana na Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema na baada ya hapo, walipewa sehemu moja ya kukaa.
Familia ya Ridhiwani ikiongozwa na Salma, mkewe Ridhiwani, wadogo zake na ndugu wengine, walikuwapo ndani ya ukumbi huo sambamba na kundi la waandishi wa habari waliofuatana nao pamoja na watu wengine 80 kutoka Chalinze.
Mgimwa alisindikizwa na watu 50 wakiwamo mama yake, mke wake na dada yake.
WAZUNGUMZIA MATARAJIO YAO
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge, Mgimwa alisema wana-Kalenga wana matatizo ya elimu, mawasiliano na kwamba tatizo kubwa ni ukosefu wa maji kwa asilimia 60.
Naye Ridhiwani alisema atatumia wadau na mashirika kuyatatua matatizo yanalowakabili wananchi ambayo serikali haiwezi kuyatatua.
SOURCE:
NIPASHE
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni