Alhamisi, 21 Agosti 2014

KAMATI KUU YA CCM YASISITIZA MCHAKATO WA KATIBA MPYA UENDELEE

Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Sekretarieti Makao Makuu ya CCM Dodoma.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Dodoma ,Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi alisema,
Kamati Kuu pamoja na mambo mengine, ilipokea taarifa na kufanya tathimini juu ya maendeleo ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini, ndani na nje ya Bunge.
Kamati Kuu vilele imepokea na kujadili taarifa kuhusu mazungumzo na mashauriano kati ya vyama vya CUF, CHADEMA, NCCR-MAGEUZI  na CCM. Mazungumzo ambayo yalisimamiwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini.
Aidha Kamati Kuu ilipokea pia taarifa ya kikao cha Baraza la Vyama vya siasa na pia taarifa ya kikao cha Kituo Cha Demokrasia nchini (TCD). Vikao hivyo vyote vilihusu maendeleo ya mchakato wa Katiba nchini.
Kuhusu mwenendo wa Bunge la Katiba, Kamati Kuu imearifiwa maendeleo ya majadiliano na upigaji kura katika kamati za Bunge hilo. Kwa ujumla Kamati Kuu imeridhishwa na namna wajumbe wa Bunge Maalum wanavyoshiriki katika kujadili na kujenga hoja na wanavyoshughulikia tofauti za kimtazamo na kimawazi katika vikao vyao na hatimaye uhutimishaji wa majadiliano kwa kura.
Kamati Kuu inawahimiza wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kuhudhuria vikao vya kamati na vile vya Bunge na kushiriki katika mijadala kwa kutanguliza masilahi mapana ya taifa na hatimae kuipatia nchi katiba inayotarajiwa na watanzania wote. Chama Cha Mapinduzi kinautakia kila lakheri mchakato huu.
Aidha Kamati Kuu imeridhishwa na juhudi za vyama na wadau mbalimbali katika kujenga na kuimarisha maridhiano na mshikamano kwa lengo la kupata muafaka. Hata hivyo Kamati Kuu imesikitishwa na kuvunjika kwa mazungumzo kati ya CCM, CUF,CHADEMA na NCCR-MAGEUZI yaliyokuwa yanasimamiwa na Msajili wa vyama vya siasa nchini kwa kengo la kujenga na kuimarisha maridhiano na mshikamano ili kupata muafaka.
Kamati Kuu imepokea na kuridhishwa na taarifa kuhusu juhudi zinazofanywa na Kituo Cha Demokrasia nchini (TCD) pamoja na vyama vinavyounda TCD katika kutafuta muafaka wa kisiasa kwa lengo la kuimarisha amani, utulivu, mshikamano na kuaminiana kati ya wadau mbalimbali na hasa kati ya vyama vya siasa.
Kamati Kuu inaunga mkono juhudi za TCD za kuendeleza mashauriano kati ya vyama na ndani ya vyama kwa lengo la kupunguza mivutano, kujenga uaminifu na ustahimilivu na umoja kati yao.
Hivyo Kamati Kuu imempongeza Katibu Mkuu wa CCM kwa namna alivyoshiriki na kukiwakilisha Chama kwenye vikao hivyo.
Kamati Kuu imemuagiza Katibu Mkuu aendelee kukutana na vyama na wadau wengine katika kufanikisha lengo la maridhiano hayo.
Mwisho Kamati Kuu inaendelea kuwasihi Watanzania wote kuendelea kushikamana na kuvumiliana pale wanapopishana kimtazamo juu ya hoja mbalimbali za katiba kwani Amani,  Utulivu na Utanzania wetu ni muhimu kuliko tofauti zetu za kimitazamo. Mchakato wa Katiba nchini uendelee kuwa fursa ya kuijenga nchi yetu badala ya kutumika kutugawa na kututenganisha.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni